Kutafsiri kati ya lugha mbili au zaidi ni kazi ambayo, hapo awali, ni binadamu pekee ambao wangeifanya. Siku hizi, inaweza kufanywa na mashine, yaani kompyuta au programu, ambayo ina uwezo wa kufanya tafsiri, yaani tafsiri ya mashine.

Natumai kwamba wengi wetu wamepata fursa ya kutumia programu kama Google Translate ambayo imeundwa kwa kazi hii. Nilipokuwa mwanafunzi wa Kifaransa, nilitegemea Google Translate sana hasa kwenye kazi za ziada zilizohitaji nitunge au kusoma hadithi za Kifaransa au kwa mazoezi ya kuzungumza na wenzangu. Katika kusoma, kila nilipopata neno ambalo silifahamu, ilikuwa rahisi sana kupiga chapa neno hilo kwenye tovuti na kupata tafsiri. Na wakati wa mazungumzo, ilikuwa rahisi zaidi kwangu kufikiria kwenye lugha ya Kiingereza kisha kutafsiri kwa Kifaransa, kwa hivyo, nilipotaka kutumia neno la Kiingereza ambalo sifahamu tafsiri yake, pia ningepiga chapa neno hili na kupata nilichohitaji.

Hali hii ya urahisi wa kutafsiri haiko sawa kwa lugha zote za dunia. Hasa tukiingia katika lugha za asili ya kiafrika, kuna mengi yasiyopo. Katika siku za hivi karibuni, nimekuwa na hamu ya kuendeleza uwezo wangu katika lugha yangu ya mama, ambayo ni mojawapo ya lugha za Kiluhya. Nimehuzunishwa sana na ukosefu wa vifaa ambavyo vingerahisisha juhudi zangu, kama katika masomo ya Kifaransa.

Kiswahili ni mojawapo ya lugha kumi na tatu za asili ya kiafrika zinazopatikana kwenye Google Translate. Lugha ya Kiswahili ina wazungumzaji wengi, takriban kati ya milioni mia moja na milioni mia moja na hamsini. Ni hali hii inayoinufaisha kwenye jukwaa za kidigitali kwani makampuni ya teknolojia hutia maanani na kujenga programu ambazo wanaamini zitatumika na watu wengi. Zaidi ya idadi ya wazungumzaji, kwa kulinganisha Kiswahili na lugha zingine za asili ya kiafrika, tunapata kwamba Kiswahili kina rasilimali zaidi ya zingine, haswa katika vifaa vya kidijitali. Pia tunapata kwamba utendaji wa vifaa hivi ni wa kiwango cha juu zaidi kwa Kiswahili, na kwa lugha zingine ambazo zina rasilimali zaidi. Hali hii imechangia kuzingatiwa kwa Kiswahili kwenye teknolojia na kwenye utafiti wa kuendeleza teknolojia hizi.

Ni muhimu kuelewa kwamba, kuwepo kwa programu ambazo zinafanya tafsiri hakumaanishi kwamba programu hizi haziwezi kufanya makosa. Kazi ambazo zinahitaji uwezo wa kufikiri, yaani zinazofanywa na binadamu, ni ngumu sana kuiga. Wataalamu wa Sayansi ya Kompyuta wanaohusiana na mada za kufunza kompyuta jinsi ya kufanya kazi ambazo kawaida hufanywa na binadamu, utaalamu unaojulikana kama Akili Bandia (Artificial Intelligence), kila siku wanaendeleza uwezo huu wa kuiga binadamu lakini teknolojia hii haijafika kiwango cha kuwa na uwezo wa kufikiria na kuchukua nafasi ya binadamu.

Katika harakati za kutayarisha makala za blogi hii, ambayo tunachapisha kwenye lugha ya Kiswahili na pia Kiingereza, nimejipata nikifanya tafsiri ya makala hapa na pale. Nikawa na hamu kujua jinsi tafsiri ambayo ningepata kutoka Google Translate ingelingana na tafsiri ambayo ningeifanya mwenyewe. Makala niliyotafsiri ni haya, “Kuwezesha Uvumbuzi wa Kiasilia katika Ulimwengu wa Kusini: Matarajio na Njia ya Kusonga mbele”.

Nilipata makosa hapa na pale ambayo ni madokezo ya mambo ambayo programu ya kutafsiri haielewi vyema.

Ya kwanza ni ngeli. Nimepata kwamba Google Translate haina uhakika au uelewano wa ngeli na jinsi zinavyofaa kuingiliana na maneno tofauti katika matumizi ya lugha.

Mfano

Sentensi katika kiingereza: This initiative aims to support local innovation approaches that are empowering and inclusive of African stakeholders.

Tafsiri ya Google Translate: Mpango huu unalenga kusaidia mbinu za uvumbuzi za ndani ambazo zinawezesha na kujumuisha wadau wa Kiafrika.

Tafsiri ya Binadamu: Mpango huu unakusudia kusaidia mbinu mpya za uvumbuzi wa kiasilia zinazowezesha na kuhusisha wadau wa Kiafrika.

Mfano huu unaonyesha kwamba programu imekosa kubadilisha ngeli ili kulinganisha na neno ‘uvumbuzi’. Programu hizi huundwa kwa kutegemea hifadhidata ya lugha, sentensi ambazo zinapatikana kwenye mtandao kwa kutungwa na wazungumzaji wa Kiswahili katika matumizi ya mtandao. Inawezekana kwamba wengi wetu katika matumizi yetu ya lugha, hatuzingatii ngeli.

Ya pili ni kuchanganya au kupoteza maana hasa sentensi inayotafsiriwa ikiwa ndefu sana.

Mfano

Sentensi katika Kiingereza: How race, nationality, and class biases limit the opportunities available to African innovators by foreign companies and investors.

Tafsiri ya Google Translate: Jinsi ubaguzi wa rangi, utaifa na tabaka unavyopunguza fursa zinazopatikana kwa wavumbuzi wa Kiafrika na makampuni na wawekezaji wa kigeni.

Tafsiri ya Binadamu: Jinsi upendeleo wa mbari, utaifa na wa kitabaka unavyowekea mipaka fursa zinazoletwa na makampuni na wawekezaji wa kigeni kwa wavumbuzi wa Kiafrika.

Mfano huu unaonyesha jinsi sentensi hii, ambayo ni refu na ngumu, inapoteza maana kabisa, kwani matumizi ya viungo vingi katika kiingereza yanahitaji umakini kutafsiri ili kuhifadhi maana.

Ni dhahiri kwamba tafsiri zinaweza kutofautiana kwa kuchagua visawe, yaani maneno tofauti yaliyo na maana sawa, na hili ni eneo lingine ambalo linahitaji umakinifu wa binadamu kudhihirisha ni neno gani linalokubalika zaidi kisemantiki.

Kwa kutamatisha, ningependa kusisitiza wazo kwamba teknolojia hizi hazifai kuchukua nafasi ya binadamu kwani haziwezi. Kwenye muktadha huu wa kufanya tafsiri, teknolojia hizi zinaweza kurahisisha kazi ya wataalamu wanaofanya tafsiri na kuendeleza juhudi zao na zetu zote kama wazungumzaji wa lugha hii tunayotamani kuiendeleza.


Maudhui yanayohusiana