Kwa miaka mingi nimekuwa nikifanya kazi na pia kujihusisha na elimu ya mtandao. Nimebahatika kusaidia Pwani Teknowgalz kupitia Africa Code Week, Mombasa Girls in STEM, Google CS Clubs, CodeHack katika vituo vya American Spaces pamoja na miradi mingine mingi. Kupitia miradi hii tulifaulu kuwashawishi na kuwavutia vijana wengi waliofurahishwa na teknolojia pamoja na manufaa yake katika maisha yao. Kutoka katika matumizi ya kawaida ya kutafuta taarifa kupitia Google, kutumia mitandao ya kijamii kuimarisha biashara na pia katika matumizi ya vifaa kama vile canva.com kutengeza michoro (graphics) ya kuvutia. Baadhi ya miradi hii ilisaidia wanafunzi kupendezwa zaidi na masomo ya sayansi pamoja na hisabati, na pia ilichangia alama zao shuleni kuongezeka. Kuna wale waliopata kazi kama vile za kusimamia na kuendesha matangazo kupitia mitandao ya kijamii na wengine kutengeza tovuti mbalimbali. Inafurahisha siku zote kuona vikao vya saa moja hadi saa mbili vinaweza kuwa na mabadiliko makubwa katika maisha ya mtu.

Mtandao umetuwezesha kufika hadi katika maeneo ya mashinani na kuandaa vikao vya kutoa mafunzo ya kimtandao. Kuna sehemu zingine ambazo ufikiaji wa mtandao ulikuwa chini lakini tulifanikisha kazi yetu. Kupatikana kwa mtandao ni changamoto kubwa ikizingatiwa kwamba tatizo la kuwapata watu walio tayari kujihusisha na uchumi wa mtandaoni. Kuna sehemu ambapo utapata ni kampuni moja tu inayotoa huduma za mtandao wa simu kwa sababu wengine wamekataa kuwekeza katika maeneo yaliyowekezwa na kampuni zingine. Hii inawalazimu watu kutumia huduma za kampuni moja tu na mara nyingi utapata kampuni hiyo inatoza ada ya juu au viwango vyao sio vya bei ya kawaida ambayo watu wote wanaweza kumudu.

Mbali na upatikanaji wa mtandao, vifaa pia ni changamoto nyingine. Katika moja ya miradi niliyohusika tulitumia tabiti (tablets) zilivyokuwa zimesambazwa shuleni humo na serikali kupitia wizara ya teknolojia na mawasiliano. Baadhi ya tabiti (tablets) hizo zilikuwa bado hazijawahi hata kutolewa ndani ya boksi zilimokuwa zimepakiwa. Uwepo wa tabiti hizo ulikuwa ni msaada mkubwa kwetu, lakini changamoto ilikuwa ni upatikanaji wa vifaa hivyo nje ya shule.

Changamoto kubwa katika miradi hii ya kutoa elimu ya mtandao ni uthabiti wa kuendesha masomo hayo. Je, washiriki wataendelea kusoma wakati tutakapoondoka? Wakati ushuru wa intaneti na muda wa maongezi ya simu utakapotiliwa mkazo itakuwa vigumu kwa watu wengi kuendelea kuwekeza katika masomo kupitia mtandao na pia kupata taarifa mbalimbali. Mbali na masomo ya mtandao pia kuna vijana wengi waliojiajiri kupitia huduma tofauti wanazozitoa mtandaoni. Wakati ambapo watu wengi hawawezi kumudu gharama za mtandao inakuwa vigumu kwa wateja kuona umuhimu wa mitandao katika biashara zao. Hatua ya kuongeza ushuru imekuja wakati mbaya, ikizingatiwa kwamba bado tunaendelea kukabiliana na janga la Uviko-19.Ongezeko hili linazidisha mgawanyiko kwa kuwanyima wengi fursa ya kugharamia mtandao. Huu ndio muda mwafaka wa vituo vya kiteknolojia ambavyo vina fedha au vinaweza kupata huduma za mtandao kwa gharama ya chini kujitokeza na kutoa huduma hii muhimu.