Alhamisi, Desemba, na joto tulivu la asubuhi linatupata jimbo la Kilifi chini ya kivuli cha mti mnene wa aina ya Mkilifi. Mahala hapa penye utulivu wa aina yake panatufanya mimi na mwenzangu tukubaliane kuwa ni mahali ambapo nasi hatungejali kuishi. Makaazi haya - kama mwelekezi wetu, Mwachiro alivyoelezea baadaye, yalijengwa mwaka wa elfu moja, kenda mia na tano- yamezungukwa na miti na mandhari ya hudhurungi na utulivu wa kupendeza, tofauti na fujo za mji wetu, Mombasa, uliojaa zege na miti michache, na tuktuk nyingi kuliko namna zingine za usafiri. Lakini tena, itakuwa ni haki kufananisha hali ya kisiwa kidogo na nyika pana iliyo na nafasi tele ambapo vijifuko vya utulivu vinaweza kubuniwa mbali na mji na fujo zake za kufikia kilele cha kufanana na miji mingine mikubwa ulimwenguni?

Wengi wetu hatujawahi kukutana ana kwa ana kabla ya hapa. Kejeli ya mitandao ya kijamii ni ujasiri wake kukufanya uhisi ukaribu wa hali ya juu na unaowasiliana nao, kana kwamba unajua kila jambo kuwahusu kupitia emoji na hisia zilizoshirikiwa. Pia mitandao ya kijamii humpa mtu chaguo la kuwa mndani na bado kuwa na marafiki kote ulimwenguni. Lakini kando na huu uwazi na desturi ya utumizi wa emoji ambazo huficha hisia zetu halisi, mawasiliano mitandaoni pia yanatumika kama kivunja-barafu na hufanya mkutano wa kwanza wa ana kwa ana kuwa wenye kuvumilika.

Lakini, kiuhakika, hakuna kinachopiku mwingiliano baina ya watu pale ambapo mawasiliano ya maneno na ya ishara zisizo na maneno huimarisha na kujenga mazungumzo yenye kufaa.

Mwenyeji wetu, Mutisya, na mwelekezi wa mkutano walitueleza kwamba dhamira ya mualiko ilikuwa kujenga urafiki na kufurahia vyakula vya pwani ya Kenya pamoja. Mkutano huu japo ulikuwa na usahali wa mjumuiko wa kirafiki uligeuka na kuwa kikao cha aina yake cha kielimu chenye kusisimua sana fikra.

Wakati tulipotulia, ilibainika wazi kuwa kulikuwa na kitu kizuri kilichokuwa kikiandaliwa jikoni. Mwenyeji wetu alitueleza kuwa tungejiburidisha na uchunguzi wake wa upishi wa chakula cha Uswahilini. Dhamira, alisema, ilikuwa kusambaza chakula cha Uswahilini ulimwenguni kwa namna utamaduni na lugha zilisafiri na chakula. Tulikuwa hapa Kilifi kutenda dhambi, saba kwa usahihi, na Mutisya aligawa vijikaratasi vilivyo fafanua chakula cha kozi saba— saba ikitokana na Imani yake ya kikatoliki— na kutuomba tuandike maoni yetu baada ya kula.

Hii haikuwezekana, na utaelewa kwa nini haya mazungumzo ya kusisimua yalitufanya pengine kama bubu vile, ama walevi, hata tukashindwa kuandika kitu kuhusu chakula cha siku.

Ratiba iliyokuwa rahisi, kila mtu kusema jina lake na kazi aliyokuwa akifanya, iligeuka mara moja na kuwa madrasa ya utamaduni. Kutoka kwa mtu wa kwanza Prof Mtanalewa hadi mtu wa mwisho, mwimbaji wa hiphop Kaa La Moto, muundo wa kiasili wa umoja wa dhamira, mahala na watu ulidhihirika. Mazungumzo yalionyesha usawa fulani— kila mtu kwa namna moja ama nyingine alikuwa anajihusisha na kuhifadhi elimu za kiasili kupitia uandishi, utengenezaji filamu, mziki, chakula, usomi na harakati za lugha. Ima kwa makusudi au mipango mingine, sote tulikuwa tumejumuika chini ya mti huu kama wanaharakati wa kitamaduni. Sadfa iliyoje, kuwa tulikusanyika chini ya mti kama vile walivyokusanyika wazee wetu miaka iliyopita kujadili masuala ya jamii.

Historia, sawa na vyombo vya lugha vinavyoisafirisha kupitia mazingira na muda, ni kitu kilicho hai na ina hali ya kujirudia. Hii sifa ya kujirudia ni kama ukumbusho wa mambo kadhaa: njia moja kama maswali— Wewe ni nani? Watoka wapi? Waenda wapi? Na kwa njia nyingine kama karipio kwa makosa yetu ya kutoieleza historiya ipasavyo, kwa kuiacha istawi katika nafasi isiyofaa ya hadithi iliyo na mtazamo wa pande moja tu, kutukemea kwa kuiendeleza kwa vizazi vijavyo kwa hali ya kutokamilika na kutokuwa na ukweli kamili. Ni namna ya historiya kuja tena kukemea na kukomboa, maana hata kwa ile hali ya usahaulifu wa kuieleza ipasavyo, lazima kutakuwa na wanaharakati katika kila kizazi wenye kupigania umuhimu wa kueleza historiya ipasavyo, na kwa mchakato huu kujikomboa nafsi na jamii zao.

Mkutano ulikuwa umepangwa kuanza kabla ya adhuhuri na kumalizika saa nane mchana, lakini bado tulikuwa chini ya huu Mkilifi karibia na jua kuzama, tukitenda dhambi saba na kuburudika na mazungumzo yenye kusisimua kuhusu umuhimu wa kuhifadhi historiya yetu ya pwani ya Kenya. Ile nafasi iliyoachwa kwenye vijikaratasi vya menyu ilibadilika na kuwa daftari, kila mmoja akiandika kutokana na mazungumzo na fikra za wengine. Kathleen, mwangalizi makini na mwanafunzi mzuri kulingana na maswali ya kutaka ufafanuzi aliyoyauliza baada ya kikao, aligawa daftari za Mozilla ambazo zilisaidia sana maanake mazungumzo yalihitaji kuandikwa zaidi.

Mwisho wa siku, matumbo yetu yakiwa yamejaa na akili zetu kusheheni maarifa tele, tulifanya mkataba. Kuwa fursa hii ya kujumuika pamoja haitakuwa ya mwanzo na mwisho na kuwa tutashirikiana kwa kazi zetu kuhifadhi historiya ya Pwani ya Kenya. Mutisya, aliyejawa na furaha kwamba tulikipenda chakula chake, na pengine kutofurahi sana kuwa tuligeuza menyu na kuwa daftari ya kuandika mengine badala ya maoni yetu kuhusu mlo, alituadhibu na kutufanya tubebe viti vilivyochongwa kutoka kwa Mkilifi, vizito kama huzuni, na kuviingiza sebuleni.

Ndizi za bokoboko bila shaka kwangu zilipendeza sana, na keki ya rasiberi ilikuwa ya aina yake duniani.


Maudhui yanayohusiana