Je umewahi jiuliza kama teknolojia ina jinsia? Na kama ina jinsia, je ni ya kike au ya kiume? Kwa haraka tunaweza sema teknolojia haina jinsia, ila mara nyingi hupendelea jinsia moja kuliko nyingine.Mara nyingi wanawake huachwa nyuma ingawa teknolojia nyingi hupewa majina ya kike kama Alexa na mengine,je hii ina athari yoyote kwa teknolojia? Kujenga teknolojia jumuishi inatulazimisha kujibu maswali haya na kutafuta muafaka wa kuhakikisha teknolojia haimuachi mtu au kundi lolote nyuma.

Katika teknolojia ya sauti, watafiti wamebaini kuwepo changamoto za kijinsia, kwa mfano, teknolojia za sauti haziwakilishi sauti ya kila mtu na tofauti zake hivyo wakati mwingine mifumo hii inashindwa kutambua sauti fulani hasa kwa upande wa jinsia na lafudhi tofauti.Ni nini kinachangia kuwepo kwa hii changamoto? Katika mradi wa Mozilla wa sauti ya jamii, tumeweza kubaini baadhi ya changamoto ambazo watafiti wamezisemea.

Kukosekana kwa data jumuishi na wazi,ni kimaanisha kutokuwepo na data zinazo wakilisha jinsia zote ili kuondoa ubaguzi katika utambuzi wa sauti.Ni vigumu kupata mgawanyo wa jinsia wa seti za data ili angalau kuonyesha kiwango cha ushiriki kwa madhumuni ya uchanganuzi wa kijinsia.Kwa upande mwingine ni ukosefu wa data wazi.Data wazi ni data ambazo ni data zinazopatikana bila malipo kwa kila mtu kutumia na kuchapisha upya apendavyo, bila vikwazo kama hakimiliki.Kuwepo kwa data zilizo wazi husaidia kukuza utengenezaji wa teknolojia mbali mbali kama teknolojia ya sauti kwani hakutakuwa na gharama za utafutaji wa data za sauti.

Teknolojia za sauti hutambua zaidi sauti za wanaume kuliko za wanawake. Hii huchangiwa pia na kukosekana kwa data jumuishi ambazo zina uwiano wa kijinsia.Utafiti wa Dkt. Tatman uliochapishwa na Sura ya Amerika Kaskazini ya Chama cha Isimu za Kompyuta (NAACL) unaonyesha kuwa utambuzi wa usemi wa Google ni sahihi kwa 13% zaidi kwa wanaume kuliko wanawake.

Upatikanaji na gharama za matumizi ya Mtandao kwa jinsia mbali mbali,katika nchi zinazoendelea wanawake wengi hawana uwezo wa kufikia na kupata teknolojia hivyo hushindwa kutumia mitandao.Upatikanaji huu ni wa aina mbili,upatikanaji wa teknolojia ya vifaa kama simu janja na pia upatikanaji wa mtandao wa intaneti wa watoa huduma hizo.Katika nchi nyingi hasa barani Africa,gharama za mtandao na vifaa zake ziko juu hivyo wanawake wengi wasio na kipato kizuri hulazimika kuchagua kati ya kula au kulipia kuunganishwa na mtandao.Kwasababu teknolojia nyingi za sauti hutumia vifurushi vya mtandao sana hivo wengi hushindwa kumudu gharama hizo.

Unyanyasaji wa kijinsia kupitia roboti ya teknolojia janja,utafiti uliofanywa na Leah Fessler wa Quartz ulibaini kuwa roboti nyingi za AI zilijibu kwa shukrani au kukubali maneno ya unyanyasaji wa kijinsia. Hii imebadilika mnamo 2020 lakini bado inaacha nafasi nyingi ya kujenga dhana potofu za kijinsia.Utafiti huu ulibaini hivi baada ya kuchunguza namna ambavyo Siri na Alexa waliitikia kuhusu maswala ya unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia.

Elimu ya kidigitali,kukosekana kwa elimu ya kidigitali huchangia kuwepo na changamoto katika upokeaji na matumizi ya teknolojia ya sauti,kwa wanawake wengi kati nchi zinazoendelea wanakosa ujuzi wa kidigitali hivyo kushindwa kutumia teknolojia ya sauti. Utafiti wa Web foundation uliolenga nchi zinazoendelea, uligundua kuwa 50% ya wanawake katika maeneo ya vijijini walisema hawakutumia mtandao kwa sababu hawajui jinsi gani. 45% ya wanawake katika maeneo ya mijini walisema hivyo.

Imani pia inaonekana kuchangia katika kutokuwa na teknolojia jumuishi kijinsia,kwani wengi hujiuliza maswali kuhusu faragha ya taarifa zao pamoja na uwezo wa kutunza taarifa zao kwa usalama.kuna wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ufuatiliaji, upendeleo, na ubaguzi na vile vile usimamizi wa data ambao unaleta hofu kuhusu viwango vya uaminifu kwa wanawake na watu wa jinsia tofauti.Wengi hasa wanawake huhofu kuwa sauti zao zinaweza kutumika visivyo na teknolojia hizi.UNESCO inapendekeza kwamba AI inapaswa kushughulikia masuala ya kibali na uthibitisho wa matumizi ya kimaadili ya data, faragha na usalama kwa wanawake na wasichana.

Ni wangapi kati yetu tunaofahamu takwimu za kijinsia za timu za wahandisi na wataalamu wanaotengeneza teknolojia mbali mbali hasa za sauti? Je tunaweza kusema kwa mfano wahandisi wa kampuni ya Google wangapi ni wanawake na wangapi ni wanaume? Kukosekana kwa takwimu hizi huchangia sana kuzohofisha ujumuishi wa kijinsia,kwani hatuwezi kujua kama mawazo na mahitaji ya jinsia mbali mbali hujumuishwa katika utengenezaji wa teknolojia mbali mbali.

Ukweli ni kwamba teknolojia haina jinsia, ni mali ya umma na kama tukiheshimia hili, tutaweza kutengeneza teknolojia inayomjali kila mtu na kumfikia kulingana na mahitaji yake.Katika mradi huu wa Mozilla, tunajaribu kujenga teknolojia ya sauti isiyo na ubaguzi wa kijinsia kwa kuhakisha kuwa tunatatua hizi changamoto.Mwezi wa kumi na mbili, tulizindua mpango kazi wetu wa jinsia utakao tuongoza kuhakikisha kuwa hatuendelezi migawanyo ya kijinsia kwa shughuli zetu.Jiunge nasi kukuza lugha ya kiswahili katika teknolojia ya sauti lakini zaidi ya yote tushirikiane kuhakikisha kuwa teknolojia ya sauti iwe ya kila mtu na sio jinsia moja tu.


Maudhui yanayohusiana