Rebecca Ryakitimbo
Wenzake wa Mozilla Rebecca Ryakitimbo

Jina langu ni Rebecca Ryakitimbo, watu wengi hupata taabu katika kutamka na kuandika jina langu la mwisho kwani ni jina lililo katika lugha ya asili ya Wazanaki. Mimi nilizaliwa katika kijiji cha Nyamuswa katika mkoa wa Musoma kisha kukulia katika mji wa Arusha uliopo kaskazini mwa Tanzania. Nilijiunga na masomo ya chuo kikuu katika Mji wa Eldoret pale nchini Kenya kusomea digrii ya uhandisi wa Teknolojia ya mawasiliano na electroniki. Wakati nikiwa katika masomo nchini Kenya niligundua kwamba wanawake wengi hawakuwa wakisomea masomo ya uhandisi na teknolojia wakiwa na mtazamo kuwa ni kazi au masomo yanayofaa zaidi jinsia ya kiume. Hii ilinipa changamoto kubwa hasa pale wengi waliposhangaa kumuona mwanamke anapanda minara ya simu na kutengeneza vifaa vya kielektroniki pale vilipoharibika. Hivyo nilipokuwa chuoni nilitumia muda mwingi na wanaume kwani nilikuwa mwanamke pekee aliyekuwa akisomea masomo ya uhandisi wa teknolojia.

Hii hali niliikuta hata nilipohitimu na kujiunga na kazi, ambapo kazi yangu ya kwanza ilikuwa katika kampuni ya kutoa huduma ya intaneti, mara nyingi watu wangeshangaa kumuona mwanamke anapanda minara na kuwarekebishia mitandao. Hapo ndipo nilipoamua kuwa maswala ya teknolojia na jinsia ni muhimu kwangu na kama mwanamke katika sekta hii inanipasa kujaribu kuwavuta wengi na kuwajuza kuwa teknolojia haina jinsia. Mnamo mwaka 2016 nikishirikiana na wanawake wenzangu waliokuwa wakifanya kazi katika sekta mbalimbali za sayansi na teknolojia tulianzisha kikundi cha TechChix. Tulitumia muda mwingi kuhamasisha wanawake na wasichana kutoogopa sekta ya sayansi na teknolojia. Kazi zetu zilipata kujulikana na hili likatuwezesha kama kundi kushinda tuzo la “Queen of Power” mnamo mwaka 2018.

Mwaka wa 2017 nilibahatika kuchaguliwa kama mmoja wa washiriki wa mkutano mkuu wa jukwaa la utawala wa mtandao katika mji wa Geneva nchini Uswisi, kule nilijifunza juu ya maswala ya utawala wa mtandao na jinsi wanawake bado wako nyuma katika maswala ya sera za mtandao. Nilichukua changamoto ile na kuamua kuleta fursa hii kwa wanawake wenzangu nchini Tanzania na Afrika Mashariki na hivyo kuwa mwanzilishi mwenza wa shule ya wanawake ya utawala wa mtandao ijulikanayo kwa lugha ya kigeni kama “Arusha Women School of Internet Governance”. Hivi sasa yapata miaka minne toka kuanza kwa shule hii, na kila mwaka tunawafikia wanawake wengine, nafurahi pale ninapoona wanawake wanajihusisha kutetea haki zao za kidijitali kama ulinzi na usalama wa taarifa zao na unyanyasaji wa kijinsia katika mitandao.

Kupitia shirika la ICANNWiki nilijifunza kuhusu kutafsiri maneno ya kitaalamu kutoka lugha ya kiingereza kwenda lugha ya kiswahili na hivyo nilipata fursa ya kuchaguliwa kuwa balozi wa shirika la ICANNWiki katika mradi wao wa kutengeneza wiki ya utawala wa mtandao kwa lugha ya Kiswahili. Ubalozi huu uliamusha upendo niliokuwa nao kwa lugha yangu ya kwanza ya Kiswahili, ikanikumbusha utoto wangu ambapo lugha ya Kiswahili ndo ilikuwa lugha iliyozungumzwa nyumbani na katika jamii iliyonizunguka kama shuleni, kanisani na hata sokoni kama lugha ya taifa. Ilinifanya kumkumbuka rafiki yangu aliyesomea katika shule ya msingi ya serikali katika lugha ya Kiswahili na kukosa bahati ya kuendeleza masoma yake hivyo lugha pekee alioyoijua ilikuwa ni Kiswahili. Nikafanya utafiti mwingi na kuona kuwa katika kurasa za mtandao kumejaa dhana na maudhui katika lugha za kigeni na sio za asili kama Kiswahili. Hivyo mimi na mwanzilishi mwenzangu wa shule hii tuliamua kuwa kila toleo la shule hii lingekuwa na madhumuni ya kutafsiri mafundisho, programu za simu na mengineyo kuwa katika lugha ya Kiswahili. Mpaka sasa tumeweza kutafsiri kupitia shule hii na kuwafundisha wanawake wa Tanzania umuhimu wa kuwa na maudhui au programu zilizo katika lugha asili kama Kiswahili hasa katika teknolojia. Mwaka juzi tuliweza kutafsiri miongozo ya usalama wa mandaoni kwa wanawake iliyotengenezwa na shirika la Internews kisha mwaka jana tulitafsiri Psiphon programu iliyowasaidia wengi kupata mawasiliano ya intaneti mwaka 2020 ambapo nchi ya Tanzania ilizima intaneti kipindi cha uchaguzi wa serikali.

Hivi sasa kupitia mradi huu wa Kiswahili katika shirika la Mozilla ninapata nafasi ya kufanya vitu viwili ninavyovipenda. Cha kwanza ni kukuza lugha yangu ya Kiswahili katika teknolojia na pili kuongeza ushirika wa wanawake na jinsia tofauti katika matumizi ya teknolojia ya sauti. Ninajua ya kwamba rafiki, ndugu na jamii zinazonizunguka hazitakosa fursa ya kushiriki katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano na teknolojia saidizi kama teknolojia ya sauti kama zikiwa katika lugha mama ya Kiswahili.

Soma zaidi kuhusu kazi ya Kiswahili hapa Mozilla:

-- Kujitambulisha, Kathleen Siminyu

-- Jina ni Britone Mwasaru


Maudhui yanayohusiana