0:00 / 0:00

Kwa jina naitwa Britone Mwasaru, mzaliwa wa Mombasa, Pwani ya Kenya. Nilijiunga na Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (Technical University of Mombasa), miaki sita iliyopita. Nilipokuwa chuoni, niliweza kujiunga na kikundi kilichokuwa kikiandaa warsha mbali mbali za kiteknolojia mjini Mombasa. Warsha hizi zilikuwa zinafanyika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta. Hapa ndipo nilipoanza kuwa na hamu ya kufanya kazi na jamii za teknolojia.

Chuoni, nilianzisha kikundi cha ufundishaji teknolojia. Tulianza kukutana mara tatu kila wiki. Tulifundishana mengi na kwa pamoja, tulijiunga na vikundi vyingine. Nilijiunga na jamii ya Swahilipot Hub na kuwa mkurugenzi wa teknolojia, cheo hichi kilinipa fursa ya kufanya kazi na wasanii mbalimbali Mombasa na Pwani nzima. Tuliandaa warsha kadha wa kadha za jinsi ya kutumia teknolojia kuuza kazi zetu kutumia mitandao ya kijamii. Wasanii wengi walitumia warsha hizi na kuanzisha blogi zao na kuandika makala. Wengi walijua jinsi ya kujiuza kupitia tovuti zao za kibanfsi. Mwaka wa 2018, niliweza kuongoza wenzagu kuandaa onyesho la uvumbuzi. Onyesho hili lilikuwa fursa ya Kenya na kila mtu kuweza kushuhudia uvumbuzi na biashara zilizopo pwani mwa Kenya. Onyesho hili liliweza kuvutia wajumbe mia sita katika muda wa wiki moja. Kupitia onyesho hili, biashara mbili ziliweza kupata uwekezaji wa dola mia tano za Marekani. Biashara hizi zilikuwa katika nyanja ya elimu na afya. Pakubwa, onyesho hili liliwapa fursa wanafunzi kutoka vyuo vikuu mjini Pwani kuja pamoja na changamoto katika mashindano ya kuvumbua vifaa vinavyoweza kutatua matatizo ya Pwani. Wanafunzi waliweza kupata zawadi na fedha baada ya onyesho hili.

Nimepata fursa ya kusaidia katika mipango kadha wa kadha zinazofanywa na kikundi cha Pwani Teknowgalz. Pwani Teknowgalz ni kikundi cha akina dada niliosoma nao chuo kikuu, ambacho kilianzishwa kuwasaidia akina dada kujiunga na nyanja tofauti tofauti za teknolojia. Niliweza kupata fursa ya kufunza akina dada walio shule za upili, vyuo vikuu, na walimu jinsi ya kufaidi kutokana na teknolojia. Pwani Teknowgalz wamenipa fursa ya kwenda sehemu za mikoani ndani ya Pwani ya Kenya, na kuweza kuonyesha na kufunza teknolojia. Kwa sasa mimi ni mshauri wa shirika lao.

Nafasi hii niliyo nayo hapa Mozilla itaniwezesha kuhakikisha teknolojia itaweza kuelewa jinsi sisi tunavyoongea na kuwezesha uvumbuzi utakaotumia lugha ya Kiswahili. Lugha huwa kizuizi kikuu cha utumizi wa teknolojia. Sio kila mtu mwenye uwezo wa kusoma na kuelewa Kiingereza, hii ni fursa nzuri ya kutumia sauti kuwezesha teknolojia kutumikia kila mtu.