Lugha ni kiungo muhimu sana katika ujumuishaji wa kidijitali. Mifumo mingi ya kiteknolojia imeundwa kutoka katika mataifa yanayotumia kiingereza kama lugha rasmi. Mbali na ugumu wa kupata vifaa pamoja na gharama zake, lugha imekuwa kikwazo kikubwa sana katika kupata huduma za kidijitali. Ni muhimu kuwepo na uwezo wa kutumia lugha unayozungumza kila siku ili kufikia au kupata huduma za kidijitali/mtandao.

Uwezekano wa kutumia lugha unayoizungumza kila siku ili kufikia au kupata huduma za mtandaoni ni muhimu na utaleta ujumuishaji mzuri wa kidijitali. Iwapo hii itafanyika hasa kwa vifaa vya viwango vya chini basi itakuwa bora zaidi. Hatua ya kuandaa na kuhifadhi lugha za kiasili katika sehemu za mashinani au katika tarakilishi itakuwa sehemu muhimu katika kufikia idadi kubwa ya watu ambao mara nyingi huwa hawafikiwi. Sauti ni kiungo muhimu katika ujumuishaji wa kidijitali/mtandao na ni muhimu kusaidia biashara zinazochipuka (startups), biashara zilizoimarika pamoja na mashirika kwenye maeneo ambapo lugha ni kikwazo. Hii ndiyo sababu naamini kuwa jukwaa au mtandao unaotumia sauti ni muhimu sana.

Hatua ya kuweka hifadhi za sauti na kuhakikisha kuwa zinapatikana kwa uwazi itasaidia katika mambo ya uvumbuzi na utafiti kwa kutumia lugha ambazo hazijazingatiwa. Hii itapunguza kikwazo kwa watu wanaojenga na kufanya utafiti wa lugha mbalimbali. Gharama za mtaji unaohitajika katika kukusanya hifadhi mbalimbali za sauti ili ziwekwe kwenye mashine za kufundishia ziko juu. Mfumo wa kijamii katika kujenga hifadhi za sauti utatoa nafasi ya kupata mchanganyiko wa taarifa (data) ambao utapunguza changamoto ya vifaa hivyo kuwa na data zinazoegemea upande mmoja.

Sauti ni muhimu lakini pia matumizi ya mfumo wa faragha/usiri kwanza (privacy first) ni muhimu zaidi. Ujenzi au utayarishaji wa vifaa vitakavyokusanya na kuandaa data za sauti unafaa kuzingatia uhifadhi wa taarifa za siri za wahusika kwanza.

Nitafurahi kuona kile kinachotengezwa kupitia data za sauti kwa kutumia lugha ya Kiswahili ambazo ziko katika mitandao mbalimbali ya mwananchi wa kawaida.