Miradi minane inayohamasisha ushirikiano wa kifedha, upatikanaji wa habari za kuaminika kwa wakulima wadogo, na haki za kisheria za mali kwa jamii zilizotengwa ndio inayopokea msaada wa Common Voice Kiswahili kwa jumla ya dola 400,000 za Marekani


KENYA, TANZANIA, NA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO | AGOSTI 22, 2022

Hili ni tambiko la kawaida. Kikundi cha wanawake wa mtaa hukusanyika Jumapili alasiri. Chai ya moto humiminwa ndani ya vikombe, Mandazi hupitishwa na salamu kwa kicheko cha kuangaza husheheni. Kila mtu anatulia - basi mazungumzo ya pesa huanza. Huu ni mkutano wa chama cha wanawake.

Chama ni ushirika usio rasmi, wa vikundi vidogo vya kuwekeza (benki ya mezani). Jina linatofautiana katika nchi tofauti za Kiafrika, lakini lengo ni lile lile - kukusanya rasilimali ili kufadhili malengo fulani. Chama kilitimiza kile ambacho taasisi nyingi za kifedha hazingeweza kukidhi: upatikanaji rahisi wa mikopo, nafasi salama ya kukusanya pesa na kubadilishana mawazo, yote yakifanywa katika lugha ya wenyeji.

Lugha ni chombo muhimu na chenye nguvu katika kutoa ufikiaji sawa wa habari. Mradi wa Mozilla wa Common Voice unashughulikia uhitaji huu kwa kuunga mkono maendeleo ya teknolojia za sauti za pamoja kwa makundi yote na jamii. Na sasa, kazi muhimu kama vile kuweka kumbukumbu/usimamizi wa Chamas, kupata taarifa za hali ya hewa zinazoaminika na zinazotegemeka, kufuatilia magonjwa ya mifugo, kupata ujuzi katika ukuzi hadi uzalishaji wa bidhaa za kilimo, na kutetea haki za wanawake za umiliki wa ardhi, zitawezeshwa kwa sauti.

Common Voice imetunuku miradi minane kila mmoja dola 50,000 za Marekani, kwa kutumia lugha ya Kiswahili na teknolojia ya sauti ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa makundi yaliyotengwa nchini Kenya, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inayozungumza Kiswahili.

Msaada huu unatolewa na Shirika la Gates kwa ushirikiano na Ofisi ya Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Kigeni (FCDO) na GIZ, kama jibu la ufahamu unaozingatia jinsia na jamii katika maendeleo ya teknolojia. Hatimaye, linakuza matumizi ya data ya sauti ya chanzo huria kwa bidhaa zinazounga mkono ushirikisho wa jamii zote katika ushirikiano.

Kuingiza lugha za watu katika teknolojia tunayounda ni hatua muhimu kuelekea kuunda teknolojia ambayo huzingatia jamii za watumiaji wa mwisho. Miradi hii imechaguliwa kwa masuluhisho yao ya ubunifu yanayogusa mambo msingi, afua za kijamii na za kiuchumi. Tumefurahishwa sana na kundi hili la washindi na kazi muhimu wanayopania kuifanya.

Anavyosema Chenai Chair, Afisa Mwandamizi wa Programu - Africa Innovation Mozilla

Programu zilichaguliwa na kamati ya uteuzi iliyoundwa na wafanyakazi wa Mozilla na mshauri wa nje wa Nairobi, Charlene Migwe- Kagume. Kagume ni Kiongozi wa Mpango wa Kikanda katika shirika la Development Gateway, aliyejikita katika kubuni na kuratibu miradi bora ya takwimu katika sekta mbalimbali.

Anasema Charlene Migwe - Kagume, Tulikuwa na shauku kubwa ya kuelewa jinsi waombaji wangebuni suluhu zinazowezekana ambazo zitashughulikia vipaumbele vilivyopo vya wakulima na kubainisha mapungufu katika mnyororo wa thamani wa kilimo. Programu nane ziliyochaguliwa ziliwasilisha mapendekezo ya kuvutia sana ambayo yalitanguliza mahitaji yanayoonekana na changamoto muhimu zinazokabili kanda.

Kutana na washindi:

Kikundi cha wanawake wakiwa wameketi wakifanya mazungumzo.

ChamaChat cha Ujuzi Craft LTD | Kenya

Mfumo wa usimamizi wa Chama wenye chatboti au programu inayoiga mazungumzo na inayoshirikisha mazungumzo baina ya wanachama na kutoa majibu ya sauti kwa Kiswahili kupitia Ujumbe mfupi (SMS)na Whatsapp. Inaunganishwa na kiolesura cha programu-tumizi ya Malipo ya kikundi, yaani API ya M-Pesa. Wanachama wanaweza kushirikiana na chatboti ya msimamizi wa Chama kwenye utendaji kazi mbalimbali, ikijumuisha kuangalia salio, maombi ya mkopo na kupokea taarifa za akaunti.

Mwanamke anashikilia viazi vitamu vya rangi ya chungwa kwenye shamba

Kiazi Bora ya Sustain Earth's Environment Africa | Tanzania

Kiazi Bora, hutumia programu ya sauti inayowafahamisha wanawake wanaoishi katika mazingira magumu na wanaoishi katika maeneo ya vijijini na jamii zilizotengwa za Tanzania kuhusu thamani za lishe ya Viazi vitamu vyenye rangi ya chungwa/njano (OFSP), ujuzi wa kilimo ili kupata mazao bora, na upatikanaji wa soko wa kina wa bidhaa za chakula ghafi au zilizosindikwa za OFSP, kupitia programu ya seti ya data ya sauti.

Picha ya simu ya zamani na iliyovunjika

Wezesha na Kabambe ya Chuo cha Westminster, U.K| Chuo cha Moi, Kenya| Chuo cha Kiufundi cha Kenya | Chuo cha Western Michigan, USA.

Ni boti ya sauti ya Kiswahili ya simu ya mkononi ambayo haitegemei muunganisho wa intaneti. Imeandaliwa kwa ushirikiano na wakulima wadogo wanawake wa vijijini nchini Kenya kama chanzo mbadala cha taarifa za kilimo. Kwa kutumia seti za data za Mozilla katika Kiswahili, boti hii ya mazungumzo ya simu ya mkononi inaweza kutumika kwenye simu za kawaida (kabambe) na simu janja na wakulima wadogo vijijini. Boti hii shirikishi ya Kiswahili inaendeshwa na hifadhidata ya maswali yanayoulizwa mara kwa mara kutoka kwa wakulima wadogo wadogo wanawake, kikundi kilichotengwa kidijitali. Imechochewa na ujuzi uliopo, kukubalika kwa teknolojia za simu katika maeneo ya mashambani nchini Kenya.

Picha ya wanaume wawili wanaomtibu ng 'ombe mgonjwa

LivHealth Kiswahili Corpus ya Badili Innovations | Kenya

LivHealth Kiswahili Corpus inalenga kuwezesha jamii kutambua kwa usahihi magonjwa ya mifugo na kupata afua kwa wakati kutoka kwa watendaji waliohitimu. Kwa kutumia Uchakataji wa Lugha Asilia (NLP), Kujifunza kwa Mashine (ML), na Akili Bandia (AI), mradi utajenga miundo ya Kiswahili ya maandishi-hadi-sauti kwa ajili ya kusambaza taarifa za magonjwa kwa jamii zilizotengwa. Wakifanya kazi kwa karibu na washirika wao, Kituo cha One Health Center in Africa(OHRECA) chenye makao yake ILRI, wataimarisha utendaji wa mfumo wa LivHealth ili kuwezesha jamii za wenyeji kupata taarifa hitajika za magonjwa kwa urahisi na kwa Kiswahili.

Picha ya wanaume wawili wakiangalia kifaa cha rununu wakati wa mazungumzo

Imarika ya Chuo cha Strathmore | Kenya

Imarika ni boti ya mazungumzo inayotoa huduma za ushauri wa hali ya hewa kidijitali katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili ambayo itasaidia wakulima wadogo kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Mradi huu unalenga kukabiliana na hatari ya wakulima kukabiliwa na hali ya hewa isiyotabirika kutokana na kukosekana kwa utabiri wa hali ya hewa unaoweza kufikiwa, wa kutegemewa na wa eneo. Upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa ni tofauti sana katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na kwa kawaida ni utabiri wa hali ya chini ya usahihi wa kitaifa au wa kikanda unaotangazwa kwenye redio na/au TV. Mradi hasa unatarajia kuwahudumia wakulima wadogo ambao mara nyingi wana ufikiaji mdogo wa huduma za ushauri wa hali ya hewa zilizowekwa ndani kutokana na vizuizi kama vile kupenya polepole kwa teknolojia au kutojua kusoma na kuandika kwa dijiti.

Picha ya nembo iliyo na kipaza sauti

Paza Sauti ya Tech Innovators Network Ltd | Kenya

Mradi huu unatengeneza boti ya mazungumzo na huduma ya mwingiliano ya mwitikio wa sauti ambayo itatoa huduma zinazowezeshwa kwa sauti katika kikoa cha usajili wa biashara na kuongeza ufahamu kuhusu matumizi ya dhamana (usalama) kuwezesha kupata mkopo nchini Kenya. Lengo kuu ni kuongeza ujuzi wa kifedha kuhusu mali zinazohamishika kama dhamana, hasa kwa wanawake katika biashara, na hasa kilimo, kwa madhumuni ya kupata mikopo. Ingawa kumekuwa na ongezeko la urahisi wa kupata mikopo, wananchi wengi bado hawajui uwezo wao wa kupata mikopo zaidi kutokana na kutumia mali zinazohamishika kama dhamana. Mradi huu utakuwa mwendelezo wa ushirikiano unaoendelea tayari na Business Registration Service - BRS (Shirika la serikali) nchini Kenya katika kikoa cha ujumuishaji wa kifedha, ambacho huhudumia umma wa Kenya.

Picha ya nembo ya shirika, inayoonyesha maandishi na sifa za utambuzi wa sauti

Kiswahili Text and Voice Recognition Platform (KTVRP) kwa Ushauri wa Kilimo na Huduma za Kifedha kwa Wakulima Wadogo ya Duniacom Group, LLC| Tanzania / Marekani

Wengi wa wakulima wadogo nchini Tanzania wana uwezo wa kuwasiliana kupitia lugha ya Kiswahili na lahaja zake pekee. Jukwaa la maandishi na sauti linalopatikana katika lugha ya watu wasiohudumiwa (yaani, Kiswahili) litakuwa ufunguo wa ufikiaji mpana, kupitishwa na matumizi ya ushauri wa kidijitali ya kilimo na huduma za kifedha nchini Tanzania. Lengo ni kuandaa jukwaa la utambuzi wa maandishi na sauti ambalo litawapa wakulima wadogo katika mnyororo wa Thamani wa Mahindi Tanzania na huduma za kidijitali za kifedha na zisizo za kifedha za kiotomatiki kwa kuzingatia eneo, maeneo ya ikolojia ya kilimo na mzunguko wa mazao. Kulingana na data iliyogawanywa kwa jinsia kutoka kwa awamu ya majaribio, inategemewa kuwa wengi wa washiriki watakuwa wanawake.

Picha ya nembo ya shirika

Haki des femmes ya Core23Lab | Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Haki des femmes itatumia teknolojia ya sauti kutoa ufikiaji wa taarifa za kisheria na usaidizi kwa wanawake katika majimbo ya Katanga na Lualaba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kuhakikisha wana haki ya kupata, kutumia, kurithi, kudhibiti na kumiliki ardhi. Wanawake wengi nchini DRC mara nyingi hupoteza uwezo wao wa kumiliki ardhi baada ya kufiwa na wapendwa wao au waume zao kutokana na kukosa ufahamu wa haki za ardhi. Suluhu hili itasaidia wanawake kupata taarifa na usaidizi wa kisheria katika kupata haki zao za ardhi kwa lugha ya Kiswahili.