Hackathon ya Kinyarwanda DeepSpeech iliyofanyika mwezi wa Februari ilihudhuriwa na watu kutoka kwa sekta ya teknolojia ya Rwanda wakija pamoja na kubuni jinsi ya kutumia API ya Kinyarwanda DeepSpeech, iliyotolewa na Digital Umuganda, kwa kazi ya utambuzi wa usemi wa Kinyarwanda. Juhudi za kuongeza Kinyarwanda kwenye Common Voice zilianza mwaka wa 2020 na sasa hifadhidata ya Kinyarwanda ni mojawapo ya zilizo kubwa sana kwenye jukwaa.
Kwa kuwa kazi hii ilitangulia kazi yetu ya kujengea Kiswahili kwenye Common Voice, kuna mengi tunayoweza kujifunza kutokana na tajriba yao na tunatumai kuboresha zaidi. Nitasisitiza mambo matatu…
1. Ushirikiano na Serikali utanufaisha Juhudi
Ilichamgamsha, na kushangaza kabisa, kushuhudia jinsi tasnia na serikali zilivyo na mwingiliano mno nchini Rwanda na jinsi makundi haya yanavyoweza kufikiana na kufanya kazi pamoja kwa urahisi. Tuligundua kwamba usaidizi wa serikali kwa mradi wa Common Voice ulisababisha kupata ruhusa wa kutumia sentensi zaidi ya milioni tatu za Kinyarwanda, na hali hii imekuwa muhimu kwa kufanikiwa kwa mradi huu.
Isitoshe, kulikuwa na mwakilishi wa serikali aliyehudhuria hackathon na kushiriki kama jaji. Kulikuwa na maoni mengi ya kujenga, mapendekezo ya kuboresha programu, washirika ambao timu zinaweza kufikiria kufuatilia nao pamoja na wale waliojitolea kutambulisha timu kwa washirika hao, baadhi ya ushirikiano huu ukiwa na taasisi za serikali. Wanasema kuwa Kigali ni ndogo na kila mtu anamfahamu mwenzake au anamfahamu mtu ambaye unahitaji kuunganishwa naye. Inafurahisha kuona hali hii ikichangia kusaidia wajasiriamali wanaoanza.
Ilichamgamsha, na kushangaza kabisa, kushuhudia jinsi tasnia na serikali zilivyo na mwingiliano mno nchini Rwanda na jinsi makundi haya yanavyoweza kufikiana na kufanya kazi pamoja kwa urahisi. Tuligundua kwamba usaidizi wa serikali kwa mradi wa Common Voice ulisababisha kupata ruhusa wa kutumia sentensi zaidi ya milioni tatu za Kinyarwanda, na hali hii imekuwa muhimu kwa kufanikiwa kwa mradi huu.
2. Utofauti katika Jamii ni Muhimu
Uzinduzi wa API ya utambuzi wa usemi wa sauti za Kinyarwanda ni hatua muhimu. Walakini, sio mwisho wa njia. Timu ya Digital Umuganda inakubali kwamba bado kuna kazi nyingi inayohitajika ili kuboresha kiwango cha utendaji wa programu hiyo. Baadhi ya juhudi hizi ni uhitaji wa kujumuisha watu tofauti katika kazi ya kuchangia hifadhidata ili utofauti huu wa jamii udhihirike kwenye hifadhidata.
Saa 2000+ za data ya Kinyarwanda zinazopatikana kwenye jukwaa la Common Voice zimechangiwa na jamii ya watu takriban elfu moja na hii inaweza kuwa sababu mojawapo ya kiwango cha juu cha makosa, kwamba utendaji wa programu sio kama inavyotarajiwa, kutokana na kiasi cha data inayopatikana.
Inawezekana kwamba kuna tofauti kubwa wa utendakazi wa programu hii kati ya mtu ambaye alikuwa mchangiaji mkuu kwenye hifadhidata na mwingine ambaye hakuchangia.
Mradi huu ulianzishwa mwanzoni mwa janga wakati mikusanyiko ya watu haikuwezekana na baadaye, ilikuwa vigumu kuongeza shauku katika mradi kati ya watu ambao walikuwa bado hawajaufahamu. Katika kazi yetu, tunatia bidii kukusanya michango kutoka kwa wigo mpana wa watu kwenye kujenga hifadhidata ya Kiswahili.
3. Wajasiriamali wanaweza na wanapaswa kumiliki Fursa za Ubunifu
Mfano wa Digital Umuganda ni mzuri na pia wa kutahadhari. Ni mfano kwamba kampuni changa imemiliki na kuendesha shughuli zinazohusu ukusanyaji wa data, kuunda programu na hatimaye kufanya kupatikana kwa API hizi kwa matumizi ya jumla ya umma. Pia wamechukua jukumu muhimu nchini wakati wa janga hili kupitia Mbaza, chatbot iliyopatikana kupitia USSD, ambayo inatoa habari muhimu kuhusiana na janga la Uviko-19. Wameingiza mapato katika mamilioni ya dola za marekani kwa kampuni za mawasiliano zinazoandaa huduma ya USSD. Walakini, mapato mengi haya huenda moja kwa moja kwa kampuni za mawasiliano...na hii ndio sehemu ya tahadhari. Hii ni dalili ya usaidizi ambao wajasiriamali wanahitaji, zaidi ya uwezo wa kiufundi/kiteknolojia. Ujuzi wa kutambua soko na kujua muundo wa mapato ambao unaweza kuwaendeleza na siku moja kuwafanya wapate faida.
Kwa kutamatisha, ilikuwa vizuri kuona moyo wa ushirikiano kati ya washiriki, wawezeshaji na majaji, wa kutaka kujenga na waliohudhuria na kuwahimiza kuendeleza kazi yao hata baada ya hackathon. Kujua zaidi ya walioshiriki na washindi, pata maelezo zaidi hapa.