0:00 / 0:00

Nina uhakika kwamba nimewahi kujitambulisha kwenye lugha ya Kiswahili, lakini yanishangaza kwamba inahisi kana kwamba ni lugha geni kwangu. Lakini pengine si jambo la kushangaza vile, kwani tangu nianze shule, nimekuwa nikizungumza sana kwenye lugha ya Kiingereza na mwenendo ukaendelea vivyo hivyo katika shule ya msingi, kisha chuo cha upili hadi chuo kikuu. Nilifunzwa Kiswahili darasani, kama wanafunzi wote wanaopitia shule zinazofuata mtaala wa elimu nchini Kenya. Lakini nje ya darasa hilo la Kiswahili, ilikuwa ngumu kunipata nikiizungumza lugha hii.

Shuleni, hasa katika miaka ambayo tulikuwa tunatarajia kuketi mitihani ya kitaifa, tungekuwa na siku maalum ya kuzungumza Kiswahili ili kututumainisha kujieleza katika lugha hii.

Katika shule ya msingi, kila Ijumaa, wakati wa mkutano wa shule, kulikuwa na nafasi ya kutuza wanafunzi kwa sababu ya vipengele tofauti. Aliyepata tuzo la Kiswahili aliitwa ‘Bingwa wa Kiswahili’ na angetarajiwa kusimama mbele ya umati wote wa shule na kusoma insha iliyomtunuku tuzo hilo. Niliwahi kulishinda tuzo hili mara moja.

Nilipofika shule ya upili, Kiswahili kilikuwa somo nililong’ang’ana nalo sana. Haikosi ni kwa sababu ya hali ile ya kutozungumza na kutoitumia lugha hii nje ya darasa. Karatasi ya fasihi hasa ndio iliyonipa msukumo sana. Mwishowe nilifaulu na kiwango hicho cha masomo na kujiunga na chuo kikuu. Nimewapa maelezo yangu binafsi ya Kiswahili kwani ingawa lugha hii inasemekana kuwa na wazungumzaji kati ya milioni hamsini na milioni mia moja na hamsini, wengi wetu tuna ustadi zaidi katika lugha za nje, kwani ndizo zinazotumika na kutiliwa maanani tunapoingia chuo kikuu na mazingira ya kazi.

Nilipojiunga na chuo kikuu, nilisoma Hesabu na Sayansi ya Kompyuta. Mwanzoni, niliridhishwa na masomo yangu yaliyohusiana na Sayansi ya Kompyuta kuliko yaliyohusiana na Hesabu, kwani kufaulu kwangu katika Hesabu kulihitaji nijikaze zaidi, yalikuwa magumu zaidi kwangu. Katika mwaka wangu wa kuhitimu masomo, nilianza kutafuta uwanja wa kitaaluma ambapo ningefanya mradi wa mwaka wa mwisho. Ilikuwa muhimu kwangu kwamba mradi huu uhusishe Sayansi ya Kompyuta kwa kiwango sawa na Hesabu, kwani nilihisi kwamba nilikuwa nimeng’ang’ana sana na masomo ya hesabu kutoyatumia. Hivi ndivyo nilivyogundua Sayansi ya Data na kuanza kuwa na hamu ya kujua zaidi kuhusu uwanja huu wa kitaaluma. Kufaulu katika mradi wangu, niliamua kufanya mfulizo wa masomo kadhaa yaliyodhibitiwa na kompyuta kwenye tovuti yaliyoandaliwa kwa kazi hii kama EdX(Edx.org) na Coursera(Coursera.org). Masomo haya yalikuwa ya bure na yaliniridhisha sana hadi nikaamua kwamba, baada ya kuhitimu masomo yangu, nilitaka kutafuta kazi kama Mwanasayansi wa Data.

Nilifanikiwa kupata kazi katika kampuni inayojulikana kama Africa’s Talking ambapo nilipata fursa ya kuendeleza maarifa yangu kama Mwanasayansi wa Data kufuatana pamoja na kazi yangu. Walinipatia fursa ya kuhudhuria mikutano na warsha yaliyoleta pamoja wakazi katika uwanja huu wa kitaaluma. Kuongeza, kwa muda wa miaka tatu nilipokuwa mfanyakazi wa Africa’s Talking, nilishirikiana na wanawake wengine waliofanya kazi hii na kuandaa kikundi kinachojulikana kama Nairobi Women in Machine Learning and Data Science kilichowasaidia wanawake wengine waliokuwa na hamu ya kujielimisha na kuingia kwenye kazi hii.

Katika harakati za kuendelea kupata maarifa, nilijipata na hamu ya kuchunguza uwanja wa kitaaluma unaoitwa Machine Learning(ML) unaohusiana kwa karibu na Sayansi ya Data. Machine Learning, kama jina la kiingereza linavyodokeza, inahusisha jinsi ya kufundisha mashine, tuseme kama kompyuta, kuweza kujielimisha kwa kutumia data na kuweza kufanya mambo kwa kujitawala, kwa mfano kuchagua kutoka picha nyingi, kadri ya mamilioni ama hata bilioni, ni gani zilizo na paka, ama zile zilizo na watu wanaokimbia. Kuna matumizi mengi ya ML yanayoenea maisha yetu ya kila siku, hususan kwa wengi wetu tunaotumia vifaa vya kielectroniki kama simu na kompyuta kushiriki katika mitandao kwenye intaneti. Kwa wale wanaotumia barua pepe, iwapo umeona pendekezo la sentensi hata kabla hujamaliza kutunga sentensi hiyo, huu pia ni utumizi wa ML.

Kwa sasa, ninafanya kazi katika uwanja wa kitaalamu unaojulukana kama Natural Language Processing, unaohusiana na mambo ya kufunza mashine namna ya kuelewa vile ambavyo binadamu wanawasiliana kwa kutumia lugha. Kumekuwa na maendeleo mengi katika uwanja huu hasa kwa lugha za nje, kama Kiingereza na Kifaransa. Lengo la juhudi zangu ni kuhakikisha kwamba lugha zetu za kiafrika haziachwi nyuma. Kazi yangu hapa Mozilla inahusisha kuunda hifadhidata ya sauti za wazungumzaji wa Kiswahili ili kutuwezesha kufunza mashine jinsi ya kuelewa na kutimika na wazungumzaji wa Kiswahili. Katika makala ya baadaye, tutachunguza faida ya vifaa hivi kwetu kama wazungumzaji wa Kiswahili.

Jina langu ni Kathleen Siminyu.

Mimi ni mkazi wa Kilifi, Kenya.

Ningependa kuweka wakfu makala haya kwa mwalimu wangu wa Kiswahili katika shule ya upili, Bi. Walela. Kwa kujihusisha kwa upendo na wema kuhakikisha kwamba sikati tamaa juhudi za kufaulu katika somo hili.

Kiswahili kitukuzwe.

~

Soma zaidi kuhusu kazi ya Kiswahili hapa Mozilla:

-- Jina ni Britone Mwasaru