Hii ni awamu ya tatu ya mashindano haya ya uandishi ambayo imeletwa kwako kwa hisani ya Mozilla Foundation. Mozilla foundation, katika juhudu zao za kuunda Kiswahili kama lugha ya mashine wameandaa hifadhi data ya Kiswahili ambayo inahusisha lahaja za Kiswahili pia, sio tu Kiswahili sanifu. Huu ni mradi ambao unastahiki kuungwa mkono kwa bidi zake za kutambua Kiswahili na Viswahili, kuwa ata kama mashine zitafundishwa lugha hii, ni muhimu kuzingatia uwepo wa lahaja na wazungumzaji wake. Kiswahili, kama wasemavyo wajuzi, kina wenyewe.

Hivi basi, hifadhi data ukiundwa kwa mtazamo huu, kuna usawa na la zaidi pia hii inakuwa ni kama namna ya kuhifadhi hizi lahaja, la sivyo zitatokomea na kusahaulika. Itakuwa kama vile miaka ya themanini na tisaini mashule mengi hapa Kenya yalivyolazimisha wanafunzi kuzungumza Kiingereza tu, na kutothamini lugha zao za kiasili. Hapo mtoto anavyoendeleza masomo yake ataitukuza lugha moja na kukosesha hadhi lugha zingine, haswa ile ya mama.

Tukithamnini siku zijazo, mradi huu wa Mozilla Common Voice ambao upo katika hali ya kujenga msingi muafaka wa hii hifadhi data, tutagundua umuhimu wa hii data na namna mashindano haya ya uandishi yanachangia kukuza Kiswahili na Viswahili kama lugha ya mashine. Na hapa tukisema ‘mashine’ tunamaanisha vyombo vyote vinavyotegemea teknolojia na namna ambavyo wazungumzaji wa Kiswahili na lahaja zake wanaweza kupata huduma, mathalan kwa simu zao, na lugha ambayo wanaifahamu vyema. Na sio huduma tu, maanake wataweza kushiriki katika shughli mbalimbali za kujijenga wenyewe na pia kuendeleza nchi kama vile kura ya maoni na kadhalika.

Mwandishi yeyote anaweza kuwasilisha kazi kwa Kiswahili na lahaja zake. Pia tunapokea kazi amabazo zimefasiriwa kutoka lugha nyingine kuja Kiswahili, na itakuwa muhimu huwataja waandishi asili. Kumbuka, kazi zitakazowasilishwa zitakuwa kwenye Public Domain (CC-0) License. Pia hatujaweka mada maalum ya uwasilishaji ili kuwapa waandishi uhuru wa ubunifu.

Mwisho wa kuwasilisha miswada ni Ijumaa tarehe 30 Novemba na washindi watatangazwa na kuzawadiwa kabla ya mwisho wa mwezi wa Desemba. Wasilisha kazi (inshaa, sio ushairi) kupitia https://forms.gle/w2yVsiJewjvmqdRo9.

Maelekezo kuhusu uwasilishaji:

  • Kazi zitakazowasilishwa zitakuwa katika public domain. Zitakuwa chini ya Public Domain (CC-0) license.
  • Idadi ya maneno ni 2500 kwa uchache na yasizidi 5,000.
  • kazi itakayopokelewa ni INSHAA/HADITHI FUPI PEKEE WALA SIO USHAIRI.
  • Uainishiaji wa maandishi:
    • Usitumie tarakimu mahala pa maneno, k.m 2021
    • Usitumie maneno ya kufupishwa, k.m “USA” au “ICE” kwa kuwa huenda yakasomwa tofauti na yanavyo tamkwa.
    • Maneno yasiwe ya kuvunja heshima.
    • Maneno yasiwe yenye kuchochea aina yoyote ya unyanyasaji au utumizi mbaya wa kijinsia
    • Maneno yasiwe ya kuendeleza dhulma au maonevu ya kijinsia
    • Maneno yaheshimu anuawai/utofauti za kijinsia, k.m matumizi ya viwakilishi vya kijinsia ifaavyo
    • Maneno yasiwe ya kuchochea vurugu/vitisho vya vurugu
    • Maneno yawasilishwe kidigitali wala sio kwa kuandikwa kwa mkono.
    • Kazi iwe yako mwenyewe.