"Je, bosi wangu anaweza kusoma ujumbe wangu wa Slack?" Ni swali la zamani kama wakati wenyewe (au angalau kama swali la zamani kuhusu mazungumzo kazini). Tunatarajia kuwepo na kiwango fulani cha faragha tunapozungumza kwenye jukwaa lolote. Lakini tunapotumia majukwaa mengi ya kidijitali kufanya mawasiliano kazini, kuna sababu ya kuwa na wasiwasi kama vile: ufuatiliaji wa mazungumzo baina ya wafanyakazi. Ikiwa umezungumza na mtu yeyote anayetumia programu kama vile Slack, Microsoft Teams au Zoom, huenda umejiuliza ni nani mwengine anayepata fursa ya kufuatilia mazungumzo haya
Jibu rahisi ni kwamba hakuna jibu hususa. Hebu tufuate orodha moja baada ya nyingine.
Je, bosi wangu anaweza kusoma ujumbe wangu wa Slack?
Kuna uwezekano mkubwa wa bosi wako kupata fursa ya kuona ujumbe wako wa Slack. Wasimamizi wanaweza kusafirisha ujumbe kutoka kwenye kituo cha mazungumzo cha umma, lakini waajiri wanaotumia toleo la bure la Slack au linalolipiwa, wanahitaji kuwasilisha ombi kwa Slack kabla ya kuona mazungumzo yako ya kibinafsi. Bosi wako atatakiwa kuthibitishia Slack kwamba ulimpa ruhusa, na ana sababu halali ya kisheria ya kuona ujumbe, au kuna “haki au sababu halali [ya kufanya hivyo] chini ya sheria husika,” hii ni kulingana na makala ya Vox kuhusu mada hiyo. Mambo huenda yakawa magumu zaidi ikiwa unafanya kazi katika sehemu fulani za serikali au ikiwa mwajiri wako analipia toleo la kiwango cha juu, ambapo mwajiri atahitajika kusoma mara kwa mara ujumbe wako na habari zingine. Programu zinginezo zinazotumiwa pamoja na Slack kama Hanzo huwaruhusu waajiri kufanya hivyo.
Unaweza kujua jinsi gani kama bosi wako anaweza kusoma ujumbe wako kwenye Slack? Nenda kwenye “[your workspace here].slack.com/account/workspace-settings#retention” ili uone ikiwa kampuni yako inaruhusu wasimamizi kufikia soga za umma na za kibinafsi ulizo nazo kwenye mfumo.
Slack, kama zana zingine tutakazotaja hapa chini, pia ina dashibodi ya shughuli ambayo inaonyesha idadi ya ujumbe ambao kila mshiriki ametuma, vituo vya mazungumzo vilivyo na gumzo sana na mambo mengineyo. Kinachokosekana kwenye Slack ni "kipengele zuizi", ili kuzuia ujumbe wa matusi kutoka kwa washiriki. Ndiyo sababu tunatoa wito kwa Slack kuweka kipengele hicho haraka iwezekanavyo. Pata habari zaidi kuhusu kampeni yetu ya #BlockAbuse na upate kuona zaidi kuhusumaoni yetu juu ya Slack juu ya mwongozo wetu mpya wa faragha usiojumuishwa wa programu za simu za video.
Vipi kuhusu mazungumzo yangu kwenye Microsoft Teams? Je, bosi wangu anaweza kuyaona?
“Lo! walio kwenye Slack hamtafurahia hilo! Unaweza kusema, "Jambo zuri mimi niko kwenye Microsoft Teams”—usijawe na shangwe haraka mno. Bosi au wasimamizi wako wanaweza kusoma ujumbe wa Microsoft Teams pia.
Kwa kufanya kazi na wasimamizi wa kampuni yako au timu ya kisheria, Microsoft inaweza kutumia chombo chake cha eDiscovery ili kufichua ujumbe wote katika Microsoft Teams, Skype, barua pepe za wafanyakazi na zaidi.
Kama Slack, Microsoft Teams inaruhusu waajiri kufichua kiasi kikubwa cha datana pia kuweza kusoma chati ambayo inatoa ripoti ya habari kama; kiasi cha ujumbe mshiriki hutuma, simu ngapi za sauti au video wamepokea, ni mara ngapi wanaanzisha mikutano na habari zaidi. Ikiwa ulihisi kama kufanya kazi ukiwa nje ya ofisi kunaweza kumzuia bosi wako kukufuatilia, fikiria tena.
Pata maelezo zaidi juu ya Hati za utambulishi za faragha za Microsoft Teams katika mwongozo wetu wa *Faragha Haujajumuishwa!
Vipi kuhusu barua pepe? Je, bosi wangu angeweza kuziona ikiwa angependa kufanya hivyo?
Tayari unajua waajiri wanaweza kufikia akaunti yako ya barua pepe ya Microsoft (kwa uwezo wa chombo cha eDiscovery kwenye Outlook pia), vipi kuhusu mtoa huduma mwingine mkubwa wa barua pepe: Google.
Ikiwa mwajiri wako anatumia Gmail, kampuni hiyo inabainisha kuwa wasimamizi wanaweza kufikia "data yoyote unayohifadhi katika akaunti hii," ambayo inaweza kujumuisha barua pepe, nyaraka, mazungumzo, na data nyingine uliyoiweka ndani ya akaunti yako ya Google ya kazini.
Kwa kifupi: usifanye au kusema chochote kwa kutumia akaunti yako ya Google ya kazini ambacho hungetarajia bosi wako hatimaye kuona!
Swali la mwisho: bosi wangu hawezi kutazama simu zangu za Zoom, sivyo?
Soga, barua pepe — vyote viwili ni njia ya mawasiliano kwa maandishi na nakala, na ni rahisi kuona jinsi vinaweza kupatikana na waajiri. Zoom, kwa upande mwingine, ni programu ya mikutano ya video. Kwa kweli mwajiri wangu hawezi kusikiliza kisiri mikutano hio, au sivyo?
Sawa?
Kwa ujumla inaonekana kama hupaswi kuwa na wasiwasi juu ya mwajiri wako kusikiliza kisiri simu zako za kibinafsi za Zoom wakati wowote hivi karibuni (hasa ikiwa unatumia nenosiri ambalo unapaswa kuwa unatumia!). Tumewasiliana na msemaji katika shirika la Zoom na amethibitisha kwamba Zoom hairuhusu watu kuingia kwenye mkutano bila kuwa mshiriki anayeonekana.
Hivyo basi, haya ni baadhi ya mambo ambayo ungependa kukumbuka.
Waajiri walio na haki za msimamizi wanaweza kusikiliza simu za Zoom zilizorekodiwa (kama ilivyothibitishwa na Reddit na msimamizi wetu wa mifumo hapa Mozilla). Ikiwa rekodi ya simu au soga zilizohifadhiwa, zimehifadhiwa kwenye wingu, zinaweza kufikiwa na wasimamizi wa akaunti. Ikiwa una wasiwasi kuhusu wasimamizi kusikiliza mikutano yako bila ufahamu wako, usijali, hawawezi kufanya hivyo.
WIRED pia inashauri kuhusu kuchagua kwa makini kile unachosema kwenye mazungumzo wakati wa simu ya Zoom. Mbali na mkaribishaji au msimamizi wa mkutano kuweza kurekodi simu, anaweza kuhifadhi kumbukumbu za soga za umma. Rekodi ya mazungumzo unayohifadhi itajumuisha mazungumzo ya kibinafsi uliyo nayo pia, kwa hivyo usimsambazie faili hiyo ya mazungumzo mtu ambaye ulikuwa ukimkejeli au kuzungumza vibaya kumhusu. Kwa kifupi, bosi wako hatimaye atapata kuona mazungumzo hayo pia.
Ikiwa unatumia programu ya simu ya Zoom, kipengele kinachoitwa ufuatiliaji wa simu kinawaruhusu watumizi walio na haki za msimamizi "kusikiliza simu bila wahusika kufahamu"—hii ni kulingana na ukurasa wa usaidizi wa Zoom. Kipengele hiki hakijawezeshwa kwa chaguo-msingi na kinaonekana kutumika tu na watumizi wa “Zoom Phone.” Ukizingatia vipengele kama “Whisper” na “Barge,” tunatumai hivyo.
Kama ilivyo katika Microsoft Teams na Slack, Zoom pia hutoa dashibodi ya shughuli kwa wale walio kwenye mipango ya matoleo ya kibiashara. Wasimamizi wa akaunti wanaweza kuona kila aina ya mambo: watumizi kumi wa kawaida, mikutano mingapi iliyofanyika, majina gani ambayo mikutano hio ilipewa, kwa muda gani ilidumu, waliokuwa kwenye mikutano hio, na zaidi. Unaweza kuona ripoti yako ya matumizi ya kibinafsi kwa kuenda kwenye sehemu ya ‘Ripoti’ ya akaunti yako ya Zoom.
Kama kawaida, unaweza kupata maelezo zaidi kuhusu Zoom katika mwongozo wetu wa *Faragha Haujajumuishwa.
Kwa hiyo naweza kufanya nini kuhusu hilo?
Tayari unajua yote kuhusu suala hili: usiseme au kufanya chochote kwenye akaunti yako ya kazi ambacho hungependa wanaochukua nafasi za uongozi kazini wajue. Lakini tunakushauri pia kuwasiliana na idara ya IT (teknolojia ya habari) ya mwajiri wako (kama tulivyofanya katika hadithi hii!) na kuuliza kuhusu sera za kuhifadhi data za kampuni yako, nani ambaye anaweza kutumia zana zipi akiwa na haki za msimamizi au ueleze tu kwamba unahangaika kuhusu suala hilo. (Watumie hadithi hii kama kisingizio, ikiwa unafikiri kuuliza moja kwa moja itakuwa vigumu!) Bosi wako huenda anaweza kujua au akose kujua lakini idara ya IT, ndio bora kuliko karibu mtu yeyote, kuweza kukupa habari sahihi.
Angalia mwongozo mpya, *Faragha Haijajumuishwa juu ya programu za simu za video. Tufuate kwenye Twitter na Instagram kwa taarifa zaidi kutoka Mozilla.